Kwanini situmii mitandao ya kijamii katika karne hii ya 21?

Reading Time: 5 minutes

Najisikia kama popote ninapoenda kila mtu anashangaa kwanini situmii mitandao ya kijamii??, ni kama vile kila mtu yupo huko lakini pia ni kama vile ni kitu cha thamani ambacho kila mtu anacho ila nikigeukiwa mimi hicho kitu sina. Nikizungumzia mitandao ya kijamii naongelea Facebook,Instagram,Snapchat na Twitter. Ilikuwa mwaka 2017, mwaka jana mwezi wa tisa ambapo nilichukua maamuzi magumu ya kujitoa kwenye mitandao ya kijamii, nilienda kutembelea Arusha ambapo nilijifunza mambo mengi lakini nilijikuta nashindwa kufurahia safari yangu kwasababu ya uwepo wa mitandao ya kijamii. Nilijikuta najilazimisha niende sehemu mbalimbali ili tu nipate vitu vya kuposti kwenye mitandao ya kijamii lakini pia sehemu ambayo natakiwa nifurahi na kuangalia maajabu najikuta niko bize kuyarekodi na kuyaposti kwenye mitandao ya kijamii. Hiyo sio sababu pekee iliyonifanya nijitoe huko lakini pia hata nakumbuka nilikuwa Uganda mwezi wa nane kwenye safari ya kimishenari, nilikuwa sijanunua kadi ya simu ya Uganda hivyo nilikuwa na ya Tanzania pekee, kwahiyo sikuweza kuwasiliana wala kuingia kwenye mitandao hiyo. Lakini nilijikuta muda mwingi nautumia kuwaza na kukumbuka lakini pia kutaka kuposti matukio niliyokutana nayo huko, kiasi kwamba nilivyorudi tu niliposti na kushirikisha safari yangu na watu mia saba na kitu niliokuwa nao Instagram lakini pia na watu elfu moja mia tano na kitu niliokuwa nao Facebook.

  
Lakini pia niligundua kuwa wakati wowote ambao nilikuwa nimeboreka nakimbilia Facebook au Instagram,kwasababu mimi sijawahai kujiunga Snapchat hadi naacha kutumia mitandao ya jamii kwasababu Twitter tayari ilikuwa ngumu kuitumia nikaona kuwa haina haja ya kuwa na mitandao mingi kwenye simu yangu hiyo niliyonayo inatosha.  Juzi nilikuwa na dada yangu ambaye yeye bado anatumia mitandao ya kijamii na nikafanikiwa kumuuliza kwanini anatumia akaniambia  akiwa ameboreka ndio anaitumia sana, lakini nakumbuka pia ushauri wa rafiki yangu ambaye hatumii mitandao ya kijamii ambapo nilimuuliza kwamba sasa nimejitoa kwenye mitandao ya kijamii nifanyeje akaniambia tafuta vitu unavyovipenda vifanye hivyo. Je inawezekana mitandao ya kijamii ni dawa? Inayotuondoa kwa muda mfupi kutoka kwenye maisha yetu au mazingira yetu yasiyotufurahisha kwa muda huo? Je inawezekana mitandao ya kijamii ni kinga? Inayotulinda na matukio yote yanayotokea mbele yetu? Je inawezekana mitandao ya kijamii ni kimbilio? Linalotusaidia kuepuka matukio halisi ya maisha yetu? 
Mwaka jana nilikaa chini na kufikiria kama bado ninataka kuendelea na mitandao ya kijamii au la, kwasababu napenda sana maisha yangu na neno linasema (Na kama jicho lako likikukosesha, ling’oe na kulitupa mbali nawe. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili- Mathayo 18:9). Kwangu mitandao ya kijamii ilikuwa hivyo, nilikuwa nashindwa kushirikiana na jamii, narudi likizo nyumbani lakini nashindwa kutumia ule muda nyumbani pamoja na familia ila muda wote nimejifungia ndani  natumia mitandao ya kijamii,  nashindwa kufanya ibada mwenyewe na kusoma neno kwasababu nikishika simu hata masaa matatu yanapita kwa siku lakini pia nisehemu ambayo shetani alikuwa akileta wivu ndani yangu juu ya maisha ya watu kwani nilikuwa nikilinganisha uzuri, maendeleo na kila kitu na watu wakati wao pia wameweka vitu vya kuigiza kwenye mitandao hiyo ila pia,nikaona kuwa ninapoelekea sio pazuri. Je unajua kuwa kila unapoenda watu asilimia kubwa wanaangalia chini kwenye simu zao, hii iliniogopesha na kunitisha kwani tumebadilisha maana ya maisha na sasa tunapima maisha yetu kwa vile tunavyoviposti, ubora wa maisha yetu ni umaarufu wetu kwenye mitandao, jambo ambalo sio zuri. Lakini pia sababu nyingine iliyonifanya nijitoe mitandao ya kijamii ni kwamba niliingia Facebook nikiwa mdogo sana, nilijiunga mwaka 2007, nilivyomaliza darasa la saba, na Instagram nilijiunga mwaka 2014, kwahiyo nilianza kutumia mitandao ya kijamii nikiwa mdogo sana na kipindi chote hicho mambo mengi yalikuwa yanatokea lakini sijawahi kuyafikiria na kuona yananiathiri kivipi ukubwani. Na hizo ndio sababu za kwanini situmii mitandao ya kijamii katika karne ya 21. Sishauri watu wajitoe kabisa kwenye mitandao ya kijamii  kwasababu hiyo ni hatua kubwa sana kwenye maisha na ni jambo kubwa kulifanya katika karne yetu hii lakini labda ni muda kuchukua mapumziko mafupi kutoka kwenye mitandao ya kijamii. Fanya uchunguzi kama mitandao ya kijamii kwako ni
  • Dawa ya kukuondoa kwenye kuboreka
  • Sehemu ya kupata kusifiwa na watu na kukubalika
  • Sehemu amabyo unaonyesha maisha yako ni mazuri kwasababu ya vitu unavyopost
  • Sehemu ya kuigiza yale maisha unayotaka na kuficha maisha yako halisi
  • Kimbilio wakati wa shida au ukiwa na mawazo
  • Sehemu unayofanya vitu visivyompendeza Mungu
  • Sehemu ya kujilinganisha na maisha ya watu na maendeleo yao
  • Sehemu unayotumia kukata kiu yako yoyote labda ya kutaka kupendwa au hisia zako zozote. Na kadharika.

Watu wengi hasa waKristo wanaweza kutumia mitandao yao ya kijamii vizuri kama vile kuhubiri, kushauria watu lakini pia kufundishia na kuonyesha mfano mzuri kwa watu wa jinsi ya kuishi. Namimi pia nilikuwa nafanya haya lakiji moyoni mitandao ya kijamii ilikuwa sehemu ya kuigizia na kuonyesha kwamba ninamaisha mazuri kwa watu kwasababu nilikuwa na posti matukio mazuri tu ya maisha yangu. Nilichojifunza ni kweli waKristo tunaweza kutumia mitandao ya kijamii vizuri lakini sio wote tumeitwa kuitumia mitandao ya kijamii kwa hivyo kwani hata enzi za Yesu hakukuwa na mitandao ya kijamii lakini alihubiri na kuwafikia watu,tusije tukawa tunatumia mitandao ya kijamii kukimbia kukutana na watu uso kwa uso kuwahubiria lakini pia tusije tukadhani kila mtu ameitwa kuhudumu kwa kutumia mitandao hiyo. Mimi ni mmoja wapo ambao sijaitwa kuhubiri huko kwani tangu nilipokuwepo kusudi langu la kuhubiri lilibadilika na la kujisifu likaja. Utandawazi usije ukatufunga tukakosa Mbingu, Yesu yu karibu kuja, kama mitandao ya kijamii inakupotezea ukaribu wako na Mungu ni heri kujitoa. Kama neno linavyosema (Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung’ang’ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu – Waebrania 12:1). Kuna rafiki yangu ambaye aliniambia aliona na kuanza kuangalia picha za ngono baada ya kuona video zinazoashiria ngono kwenye Instagram na baadae akaja kuanza kujinasua kutokana na addiction hiyo,kama mitandao ya kijamii inakuingizia chuki,wivu,hasira na dhambi zinazokunyemelea kama picha za ngono na kadharika ni heri kujitoa , ili vitu vidogo vidogo kama hivi visijekukukosesha Mbingu. Ni heri kuonekana mshamba kwa watu ila sio kwa Mungu. Kwahiyo kama unaona haikuongezei katika ukuaji wako wa kiRoho ni heri kujitoa.

Ubarikiwe.

Maombi: Baba Mungu ninakuja mbele zako kukushukuru kwaajili ya kuzaliwa katik karne hii yenye maendeleo ya 21, ninakushukur kwasababu upo, na unanilinda. Ninakuja mbele zako nikiomba rehema  na msamaha palo kote nilipokwenda kinyume na mapenzi yako kwasababu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, ukanifute katika kitabu cha hukumu na kuniandika katika kitabu cha uzima wa milele. Lakini pia ukanisaidie kufanya maamuzi na hii mitandao ya kijamii niliyonayo sawasawa na mapenzi yako kwaajili ya maisha yangu,ni katika Jina lipitalo majina yote la Yesu,AMEN.

 

Related Posts

One Reply to “Kwanini situmii mitandao ya kijamii katika karne hii ya 21?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *