Unapopitia magumu… (Sehemu ya Tatu).

Reading Time: 3 minutes

Nimepata habari za msiba, rafiki yangu wa karibu amefiwa na dada yake, nimeumia sana. Kwanza kwa sababu habari nilizozisikia zinaumiza sana, na najua wanapita kipindi kigumu japokuwa sijaubeba mzigo aliobeba yeye lakini naamini ni mzito. Ushawahi kufikia kipindi ambacho hakuna kitu ambacho mtu anasema kitaelezea maumivu yako kwa undani? Au labda uko katika kipindi hicho sasa? Ushawahi kuwa katika kipindi ambacho maumivu ni makubwa na hauna maneno ya kuyaelezea ili mtu aelewe, ushawahi kuumia mpaka ukahisi ni heri ungezaliwa kipindi kingine katika hii dunia ili usizione hizi siku unazopitia? Au ni sasa ndo unaumia na kujisikia hivyo? Najua umepitia,unapitia au utapitia magumu, na natamani niwe na maneno ya kukuambia ambayo yataondoa maumivu yako kabisa, napenda nikufariji mpaka ukasahau tatizo lako lakini siwezi, kwa maana mimi pia ni mwanadamu ambaye maneno yangu yana mwisho wa kubeba uzito.

Wakati unapitia kipindi kigumu, sikusema haya yanaondoa magumu unayoyapitia ila yatakusaidia katika kipindi kigumu hicho mpaka utakapovuka. Nikukumbushe ujapo pita kati ya bonde la uvuli wa mauti, bado Bwana yu pamoja  nawe hata hapo, ujapokuwa chini zaidi ya nchi au juu zaidi ya mawingu, bado yeye yupo pamoja nawe. Ujapokuwa gerezani, utumwani,mahututi kumbuka hajakuacha,hakuachi, hatokuacha,yu pamoja nawe mpaka mwisho.

Leo ningependa kuongeza vitu vilivyonisaidia wakati napitia magumu, ambavyo nawewe unaweza kuvifanya, kwa vitu vilivyopita nilivyovitaja unaweza kuvipata kwenye post zilizopita, lakini leo nina mengine ya kuongezea, nayo ni:

 1. Tafuta nyimbo inayoelezea ushindi katika hali unayoipitia: mara nyingi nimejikuta kuna nyimbo ninayoiimba ambayo inaakisi matukio yanayotokea kwenye maisha yangu,nakumbuka wakati niko Arusha nilikuwa nikiimba wimbo wa Darlene Zschech (hapa) ambayo ni nyimbo inayokiri uponyaji, na bila kujua nilikuwa nakiri uponyaji kwa ajili ya mama yangu. Naomba nikushirikishe nyimbo mbalimbali ambazo zilinisaidia  kukiri ushindi katika vipindi vigumu mbalimbali katika maisha yangu. Lakini pia kama unanyimbo zako zilizokusaidia  kukiri ushindi katika kipindi unachopitia ambacho hata kuelezea magumu yako vizuri hauwezi,ningependa kuzijua pia.

 Zifuatazo ni nyimbo ambazo zitakutia moyo katika kipindi kigumu:

  Hizo ni nyimbo chache ambazo zimenifariji kwenye magumu, na zinaendelea kunifariji na kunitia nguvu ninapoelekea ushindi, nakuombea pia zikuhudumie na uendelee kukiri uponyaji na ushindi ktika magumu unayoyapitia.
    
   2. Tamka mambo chanya kwenye maisha yako na katika kipindi hicho: Najua maisha yanapoleta shida jambo la mwisho ambalo unatamani kulifanya ni kutamka mambo chanya,kwasababu tuseme ukweli mambo tunayoyapitia muda mwingine yanatufanya tusitamani kuishi au kuongea mema juu yetu na maisha yetu, lakini tukumbuke kuwa kwenye vinywa vyetu kuna nguvu ya kuhuisha na kuua, tutumie vinywa vyetu vizuri hasa katika kipindi kigumu.Ongea mambo mazuri na unayoyataka kuyaona katika kipindi chako, tamka uzima katika magumu yako, usiache kujizungumzia vizuri katika maisha, kinywa chako kina nguvu sana lakini hii ni topic ya siku nyingine.

    3. Soma Neno la Mungu sana katika kipindi hiki: hasa katika vitabu vinavyoonyesha watu waliopitia majaribu na jinsi Mungu alivyoonekana kwao na kuwashindia. Ayubu,Daniel, Paulo na watumishi wengi walipitia majaribu lakini waliyashinda. Soma sana Neno katika kipindi hiki najua kitu cha mwisho unachotamani kukifanya ni kusoma Neno lakini nakuahidi kuna nguvu katika kuona wenzio wanakombolewa katika magumu yao, na kumtazama huyo Mungu aliowafanyia hao na wewe kuwa na tumaini la kwamba nawewe atakufanyia.

    4.Sikiliza shuhuda: Shuhuda zinajenga,shuhuda zinakuvusha sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Ufunuo 12:11- “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”. Nakumbuka dada yangu mmoja tulikuwa tunashirkiana mambo mbalimbali na akawa ananiambia kwamba alikuwa amevunjika moyo lakini alienda kwenye ibada na akasikia mtu anatoa ushuhud ambao ulimvusha mpaka akajiuliza kama Mungu anawafanyia hawa je si zaidi mimi.

    5. Pingana na woga wako: Neno linasema  ”  Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.”- 2 Timotheo 1:7. Kwahivyo muda wowote tunaosikia woga tukumbuke haukutoka kwa Mungu kwa maana Mungu hakutupa Roho wa uoga, pingana na woga wako, kuwa na msimamo katika Roho mwenye kutujalia nguvu tuliopewa, simama kama Daniel alivyosimama, kama Meshack, Abednego na Shadrack walivyosimama kwa ujasiri. Pingana na woga, kila utakaposikia maneno ya kukutia woga, pambana nayo. Usimwache shetani awe ni msemaji wa mwisho kwa kukuachia woga.

  Kwa leo naomba niishie hapa, lakini nitamalizia kuhusu mambo mengine zaidi kwenye Sehemu ya Nne ambayo itakuwa ya mwisho.

   Ubarikiwe.

  Maombi: Mungu mfariji wetu, naomba kwaajili ya watakaosoma hii blogpost, Wewe unajua hali wanayoipitia, Wewe ni mkombozi na Baba yetu, naomba ukapate kuwa fariji, kuwavusha na mkono wako wenye nguvu sana ukawaokoe katika hali zote, na mateso yote, Jina lako likatukuzwe katika maisha yao,AMEN.

  Related Posts

  Leave a Reply

  Your email address will not be published. Required fields are marked *