Faith Talk

TUONGEE : Kumuamini Mungu

Reading Time: 4 minutes
               Warumi 10:17- Basi imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Umeshawahi kupitia jambo na kipindi hicho cha mapito ukaishiwa nguvu za kuamini kuwa Mungu anaweza kukuokoa katika hilo? Umeshawahi kuwa katika tatizo ambalo toka uzaliwe haujawahi kulipitia na ukashindwa kuamini kwamba Mungu anaweza hata hapo? Umeshawahi jaribiwa mpaka ukashindwa kumtukuza Mungu hata katikati ya jaribu? Ushawahi kuumizwa mpaka ukaona Mungu hayupo? Ushawahi kuteseka mpaka ukamkataa Mungu na ukatamani kufa? Ushawahi kujaribiwa kwa muda mrefu mpaka ukahisi hilo ni jaribu lako mpaka kifo? Na je umeshawahi kupitia kipindi ambacho unaamini Mungu anaweza, ila kila ukiomba hauna imani kwamba anaweza katika hilo, lakini pia moyo wako unazimia kuamini kwamba mema yatatokea,ni kweli unaomba na unajua Mungu anaweza lakini kila saa woga unakushinda na unashindwa kuamini kwamba anaweza kukuvusha, ni sawa na unaomba kitu kimoja na unaamini utapata kitu kingine… Napenda kukuambia hauko peke yako. Namimi pia huwa napitia vipindi hivyo. Vipindi ambavyo unadhani dunia imeisha kwa upande wako,vipindi ambavyo unahisi kwamba ikitokea matokeo mengine dunia yako yote itasimama,vipindi ambavyo unahisi maisha yako yanategemea matokeo ya jaribu lako, lakini pia vipindi ambavyo unajiuliza kama kweli Mungu yupo, na kama yupo je anasikia maombi yangu? Na kama anasikia, inawezekana Yuko kimya kwasasa. Vipindi ambavyo ukiwaza tu jaribu lako mwili wako unaishiwa nguvu na kutetemeka.

Woga huwa unanishangaza sana, unauwezo wa kukufanya usahau kule Mungu alikokutoa
Na ndio njia ya shetani anayoitumia kutufanya tusimuamini Mungu katika haya ya sasa, kwasababu anatufanya tusahau kwamba Mungu ametuvusha katika mengi kabla ya hili. Woga unauwezo wa kukufanya uzimie moyo pale tu unapowaza jambo unalopitia, una uwezo wa kukufanya kutetemeka mtu anapotaja jaribu lako, woga unanishangaza sana. Unakufanya uhisi uko peke yako duniani, na Mungu hayupo, na kama yupo basi yupo mbali sana na jaribu lako. Na ndio maana Neno linasema hautoki kwa Mungu kwasababu unatusababisha kuona Yeye hayupo katika matatizo yetu, na kukuza matatizo yetu kuliko Jina la Yeye anayeweza kutuokoa. Mungu hakutupa roho ya woga (2 Timotheo 1:7-Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi). Woga unatufanya tumkosee Mungu na kushindwa kumuamini katika tunayoyapitia, na kuhisi Yeye hawezi, na kumuondoa katika ukuu wake mioyoni mwetu na kuweka ukubwa wa matatizo yetu. 

Waebrani 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
Natamani nimuamini Mungu sana katika maisha yangu na nisimpe nafasi shetani ya kuiondoa imani yangu kwake, lakini kuna muda unapitia mambo ambayo unahisi kushindwa kumuamini Mungu katika hilo jambo. Ningependa nikushirikishe jinsi mimi ninavyojitia moyo na kurudi kumuamini tena, kuamini nguvu zake katika maisha yangu na kujua kwamba anaweza, na kujikumbusha kwamba kama aliweza zamani zile anaweza hata leo.

Nasoma Neno

Imani huja kwa kusikia, Neno la Mungu. Neno la Mungu hutupa nguvu ya kuyavuka majaribu kwasababu Neno la Mungu li hai, unaweza kusoma kuhusu umuhimu wa kusoma neno la Mungu hapa. Lakini ukisoma na ukaona jinsi Mungu alivyofanya zamani na ukajikumbusha jinsi alivyokutoa kwenye mambo mbalimbali, imani yako inainuka ndani yako na kuamini kwamba anaweza kufanya na unazidi kuamini.
Namwachia Mungu
Kumwachia Mungu kunaonyesha jinsi gani unaamini utendaji kazi wake, na unaamini kwamba Yeye ni muweza wa yote. Kumwachia Mungu sio swala ambalo unasema kama vile waswahili tulivyokuwa na msemo kwamba namwachia Mungu, ila inahusisha maombi, na kuliondoa swala katika mawazo yako katika kujaribu kutafuta ufumbuzi mwenyewe. Kwanza ni kuomba na kuliacha mikononi mwa Mungu, lakini pia kuacha kujaribu kutafuta ufumbuzi mwenyewe wa hilo swala, unaweza ukasema umemwachia Mungu lakini kichwani bado unatafuta njia za kujikomboa kwa akili  za kibinadamu, kama umeomba na ukapata mwongozo wa kufanya hivyo fanya, lakini kama haujapata mwongozo tulia. Kutoka 14:13-14 “ Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya”.
Naabudu
Nilishangazwa sana na Ayubu wa kwenye Biblia, katika habari zote alizozisikia alichokifanya baada ya kuambiwa hayo yote ndo kilinishangaza, “Ayubu 1:20- Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu”. Woooow, ni mara ngapi tunapopitia mambo magumu au tunapopata habari mbaya tunafanya alivyofanya Ayubu? Na sisi wengine hata tukipata habari njema kimbilio letu ni kuwaambia watu na kufurahia lakini hatufanyi kama alivyofanya Ayubu. Unazidi kumuamini mtu uliye karibu naye, kwasababu unamjua sauti, mwenendo na unamjua alivyo, ndivyo hivyo unazidi kumuamini Mungu ambaye unamuabudu na upo karibu naye. Unaweza kumuamini Mungu zaidi Yule ambaye unakaa naye kwa ukaribu, kwa kumuabudu. Abudu,imani yako itaongezeka.
Tamka yale unayotaka yatokee
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, unatarajia nini kutoka katika hilo unalolipitia? Tamka hilo, ongea hilo. Usitarajie kingine na ukawa unatamka kingine.  Waebrania 11:1-“ Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” 
Je upo katika kipindi kigumu ambacho unashindwa kumuamini Mungu? Je tatizo lako linakuchosha sana kiasi unasahau ukuu wa Mungu? Nikukumbushe Mungu yuko juu na duniani ni mahali pake pakuwekea miguu (Isaya 66:1-“Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? “), tatizo lako Kwake ni dogo sana. Liko chini sana kiasi kwamba halimshtui, halimuogopeshi na anaweza katika yote Yeye anauwezo na anacontrol mambo yote, hakuna linaloweza kutokea katika maisha yako ambalo litamuogopesha au kumshtua, na Yeye ndiye Baba yako, ana majibu ya matatizo yako, na Yeye ndiye anayeweza kubadilisha hali yoyote unayoipitia, usiache kumuamini.
Ubarikiwe,
Eunice?
 

Follow Eunice on Instagram 💜

24, proud Tanzanian, taking life one day at a time and being less judgmental on this amazing journey. I haven't figured out everything in life, and i am okay with that.

One Comment

Leave a Reply

%d bloggers like this: