Sababu 11 za Kibiblia za kwanini unahitaji kushirikiana na watu kwenye maisha yako.

Reading Time: 2 minutes

“Kujiamini sio vibaya ila muda mwingine ule utu wetu wa ndani unajisikia sana kiasi kwamba tunasahau bila Mungu na bila watu aliowaweka kwenye maisha yetu tusingekuwa hapa tulipo.”

Katika dunia ya sasa ambayo watu wanajisifu kwakutimiza au kuweza vitu kwa nguvu zao wenyewe nimeshangazwa sana kusoma mistari mbalimbali kwenye Biblia inayotushauri na kuhamasisha umoja na ushirikiano na wengine katika maisha yetu ya kila siku. Baada ya kuandika sehemu ya kwanza ya kwanini tunahitaji watu kwenye maisha yetu ambayo unaweza kuisoma hapa.  Nimeona nielezee Biblia inasemaje kuhusu kushirikiana na nafasi ya watu kwenye maisha yetu. Ili tusiishi kama tunajitosheleza wakati Mungu ameweka marafiki katika maisha yetu kwaajili ya utukufu wake kwetu.

Na hii ni mistari kumi na moja inayoambatana na sababu za kwanini kushirikiana na wenzetu au watu Mungu aliowaweka kwenye maisha yetu ni muhimu:

 1. Kila mmoja ni kiungo cha mwenzake- Warumi 12:5, “vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.”
 2. Kushirikiana na wengine kunakupa nafasi ya kuhusika katika hali zote za maisha za wengine kama Kristo alivyotuonyesha mfano- “Warumi 12:15, “Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao”.
 3. Kila mmoja wetu amejaa mambo mazuri ndani yake ambayo yanaweza kutufaa kwa kuonyana na kutupa maarifa- Warumi 15:14, “Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana.”
 4. Kwaajili ya kushirikiana na kuondoa utengano na kupata faida mbalimbali za kushirikiana kama nilizozitoa hapa pia- 1 Wakorintho 12:25, “ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane.”
 5. Unahitaji kushirikiana na watu kwasababu ya kufarijiana kwa mambo mbalimbali tunayopitia kwenye maisha, mara nyingine jaribu unalopitia kuna mtu kashalivuka hivyo ushauri wake unaweza kukujenga lakini mara nyingine uwepo wa watu ambao wanaweza kupitia jambo fulani na wewe unasaidia kukufariji- 1 Wathesalonike 5:11.
 6. Kushirikiana na wengine kunaonyesha pendo tulionalo kwa Kristo- Waefeso 5:21,” Kila mmoja wenu ajinyenyekeze kwa mwenzio kwasababu ya upendo mlio kuwa nao kwa Kristo.”
 7. Kushirikiana kunakusaidia kukuza matunda ya Roho ndani yako, unajifunza upole, unyenyekevu na uvumilivu- Waefeso 4:2.
 8. Kushirikiana na watu kunakujenga kuwa mtu bora anayefanana na Kristo lakini pia kunakusukuma kutenda mema- Waebrania 10:24,”Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.”
 9. Mungu ametujalia vipawa mbalimbali, kushirikiana na wengine kunatuwezesha kutumia vipawa vyetu kwaajili yao lakini pia kwaajili ya kanisa- 1Petro 4:10,” Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.”
 10. Kushirikiana na watu kunakusaidia katika kupata maombi ya wengi lakini pia kupata watu ambao unaweza ukaungama dhambi zako kwao na wakakusaidia ukaponywa au kuvuka katika hilo eneo- Yakobo 5:16
 11. Katika dunia ambayo inamambo mengi yanayoendelea kuwa na watu wanaoweza kubeba mizigo yako, maumivu yako na shida zako kama zao ni jambo zuri sana- Wagalatia 6:2,”Chukulianeni mizigo yenu; na kwa njia hiyo mtaweza kutimiza sheria ya Kristo.

Wakati wowote utakapojisikia hauhitaji kushirikiana na wengine katika safari yako ya maisha, jikumbushe umuhimu wa kufanya hivyo kutoka kwenye Neno la Mungu. Na Mungu atusaidie kuenenda hivyo japokuwa kuna mambo mengi yanayoambatana na kushirikiana na watu lakini naamini katika yote Mungu anamakusudi na mipango yake katika yote lakini zaidi ya yote analeta watu kwenye maisha yetu kwa mipango yake.


Ubarikiwe,
Eunice?.

Related Posts

One Reply to “Sababu 11 za Kibiblia za kwanini unahitaji kushirikiana na watu kwenye maisha yako.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *